Ripoti hii ni matokeo ya utafiti uliofanywa na Amnesty International kuhusu matendo ya serikali ya Tanzania ambayo yalisababisha Wamaasai kuhamishwa kwa nguvu Loliondo. Kimsingi, inaangazia ukiukwaji wa haki za binadamu wakati wa zoezi la kuwahamisha kwa nguvu la Juni, 2022, lakini pia inaangalia historia ya ukiukwaji mwingine wa haki za binadamu na ubaguzi dhidi ya watu wa Loliondo, ambao ulisababisha matukio ya Juni 2022. Ripoti hii inaonesha kwamba ukatili ulitumika dhidi ya Wamaasai kuchukua kilomita za mraba 1,500 za ardhi ya vijiji vya Loliondo na inaonesha mapungufu makubwa katika mchakato wa kutoa maamuzi yaliyotumika kuhalilisha uhamishwaji kwa nguvu uliofanyika. Hii inajumuisha matukio mbalimbali ya uhamishaji kwa nguvu ya mwaka 2009, 2013, 2017 na 2022 yaliyofanywa na vikosi mbalimbali vya majeshi ya usalama, kwa kushirikiana na wawakilishi wa kampuni binafsi inayoendesha shughuli zake Loliondo, katika matukio yote. Pia inaonesha jinsi gani serikali inaendelea kuwatenga wanajumuiya ambao wana haki kwenye ardhi na ndiyo wasimamizi wa ardhi katika mipango yake ya uhifadhi, na badala yake inawaondoa katika ardhi yao ya asili ya ufugaji, na kuwakataza kutumia rasilimali zilizopo katika ardhi yao ya malisho na kutotoa fidia yoyote kwa jambo hilo.

